Polisi mkoani hapa wanamsaka mwanamke ambaye aliyejifanya muuguzi na kuiba mtoto wa kike wa siku moja kwenye wodi ya wazazi katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya.
Mtoto huyo alizaliwa kwa njia ya upasuaji na Sarah Mwasanga (40), mkazi wa Iganzo jijini hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohamed Mpinga alisema tukio hilo lilitokea juzi alfajiri kabla ya ndugu na jamaa kuingia kuona wagonjwa.
Mpinga alisema mwanamke huyo alifika hospitalini hapo kwa pikipiki huku akiwa amebeba kitu mithili ya mtoto na alipohijiwa na walinzi getini, alieleza ana mgonjwa ameandikiwa sindano za masaa hivyo akaruhusiwa kuingia.
“Alitumia mbinu ambayo kwa namna moja au nyingine ilifanikisha azma yake jambo ambalo hata wakati anatoka walinzi hawakumtilia shaka kwa kutambua tayari kapatiwa huduma,” alisema.
Mpinga alisema awali alipoingia kwenye wodi ya wazazi, aliwahoji kinamama waliojifungua kuwa anahitaji mtoto wa kike kwa ajili ya kumpatia chanjo, ndipo mzazi wa mtoto huyo alimkabidhi kwa kutambua ni muuguzi kutokana na mavazi aliyokuwa amevaa.
Alisema hilo ni tukio kubwa lililotokea mkoani hapa tangu aliporipoti na kwamba wanaendelea na uchunguzi.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Yahaya Msuya amekiri kutokea kwa tukio hilo, na kwamba kwa sasa lipo kwenye uchunguzi zaidi.
Mama wa mtoto huyo, Sarah Mwasanga aliomba msaada wa jeshi la polisi kufanya jitihada za haraka kuhakikisha mtoto wake anapatikana.
No comments:
Post a Comment