Okwi, Bocco wapewa timu - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Thursday 18 January 2018

Okwi, Bocco wapewa timu

MCHAWI mpe mwanao akulelee ili awe salama. Hiki ndicho ambacho kimefanyika Msimbazi ambapo benchi la ufundi la Simba linatarajia kufanya maamuzi magumu ya kukabidhi timu hiyo kwa wakali wawili, Emmanuel Okwi na John Bocco.

Okwi hakuwa na timu tangu mwishoni mwa Novemba mwaka jana kutokana na majeraha ya enka pamoja na utoro, lakini Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Masudi Djuma, amesema Mganda huyo sasa yuko fiti na huenda akacheza mchezo wa leo Alhamisi dhidi ya Singida United.

Kinara huyo wa mabao anatarajiwa kuanza sambamba na Bocco katika safu ya ushambuliaji, kusaka ushindi muhimu dhidi ya Singida inayonolewa na kocha bora zaidi nchini, Hans Pluijm.

Djuma ameweka wazi alimpa Okwi sharti la kuomba msamaha kwa wachezaji wenzake kwa kuchelewa kujiunga na kambi na tayari amefanya hivyo.

Mbali ya kuwaomba msamaha wachezaji wenzake, Okwi pia alilazimika kumwelezea kocha huyo kilichomfanya achelewe kujiunga na kambi hiyo tangu alipoumia mwaka jana.

Baada ya kuomba msamaha na kusamehewa Djuma aliweka wazi atamtumia Okwi katika mechi ya leo kwani hana kinyongo na hajawahi kuwa na vinyongo na wachezaji.

“Nimemsamehe Okwi na wenzake wamemsamehe baada ya kuwaomba msamaha pia, hayo ndiyo maisha ninayoyataka ili kujenga umoja ndani ya timu,” alisema kocha huyo aliyechemsha katika Kombe la Mapinduzi.

Mechi yenyewe
Mechi ya leo inaonekana kubeba hatma kubwa ya timu zote mbili ambapo endapo Simba itashinda itakuwa imejiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara huku Singida nayo ikipambana kupanda nafasi mbili za juu.

Simba inaongoza ligi kwa wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa kwani ina pointi 26 sawa na Azam iliyoko nafasi ya pili.

Singida ipo nafasi ya nne na pointi 23. Djuma alisema baada ya kupata matokeo mabaya kwenye michuano ya Mapinduzi na FA, wamerejesha akili yao kwenye mechi za Ligi Kuu na leo watapambana kuhakikisha wanaondoka na alama zote tatu.

“Singida ni timu nzuri, nimewaona Mapinduzi walicheza vizuri, ila hata katika ligi pia wamefanya vizuri ndio maana wapo katika timu za juu. Lakini nitahakikisha tunapata pointi tatu dhidi yao kwani hatuna la kupoteza tena,” alisema Djuma.

Kocha Pluijm alisema wanawaheshimu Simba kuwa ni timu kubwa na wataingia katika mechi hiyo kwa nidhamu zaidi.

“Lengo letu ni kutwaa taji, tunataka kushinda mechi zote, sio hii tu dhidi ya Simba. Maandalizi yetu yamekwenda vizuri na tutapambana kupata ushindi,” alisema.

No comments:

Post a Comment