Naibu meya ukawa awavuruga CCM - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Tuesday 9 January 2018

Naibu meya ukawa awavuruga CCM

Baadhi ya viongozi wa CCM wameendelea kutuhumiana kuhusu hatua ya mmoja wa wajumbe wa chama hicho kumpigia kura mgombea wa unaibu meya wa jiji la Dar es Salaam kwa tiketi ya Ukawa.

Uchaguzi huo, uliokuwa na mchuano mkali kwa kila upande kuwa na wajumbe 11 kwa 11 ulifanyika Januari 3 katika ukumbi wa Karimjee na Mussa Kafana wa CUF aliibuka kidedea kwa kupata 12 dhidi ya 10 alizopata Mariam Lulida wa CCM.

Baada haya ya matokeo hayo siku iliyofuata mjumbe baraza hilo CCM, Abdallah Chaurembo ambaye pia ni Meya wa Temeke alisema wapo katika hatua za mwisho kumtambua aliyesababisha wao kushindwa uchaguzi huo na kwamba ushahidi wanao na wameshaanza kumbaini.

Lakini jana Jumatatu, Mwenyekiti wa Jumuiya wa Vijana wa CCM (UVCCM), Wilaya ya Kigamboni, Mponela Mathei alimtaka meya wa manispaa hiyo, Maabadi Hoja kukaa pembeni ili kupisha uchunguzi kwa kuwa ni mjumbe anayedaiwa kuwapigia kura wapinzani katika uchaguzi huo uliokuwa na mchuano mkali.

Mathei alisema wamefikia hatua hiyo, baada ya Wilaya Kigamboni kunyooshewa kidole baada ya uchaguzi huo kumalizika na kila mwanaCCM anamtaja meya huyo ambaye pia ni diwani wa Pemba Mnazi.

“Ingawa kura ni siri, lakini tunamuomba ndugu Hoja akae pembeni ili kupisha uchunguzi dhidi yake. Taarifa tulizonazo na ushaidi tulioukusanya zinamlenga yeye na kwa nini zisimtaje wajumbe wengine kama Dk Ndugulile (Faustine) na mwenzake, lakini kila mtu anamtaja meya huyu,” alisema Mathei.

Alisema ingawa jambo hilo linashughulikiwa ngazi ya juu ya chama hicho, umoja huo umeona usikae kimya badala yake umetoa tamko la kulaani kitendo hicho kinachodaiwa kufanywa na meya huyo ambaye hadi sasa hajaeleza lolote kuhusu tuhuma hizo.

“Sisi tunamsaidia kumaliza suala hili, ndiyo maana tunamtaka akae pembeni ili kupisha uchunguzi dhidi yake na kama haitathibitika itajulikana tu, lakini ukweli ni meya huyo anatajwa sana tangu siku ile kabla ya uchaguzi na baada ya kumalizika,” alisema Mathei.

Akizungumzia tuhuma hizo, Hoja aliushangaa umoja huo na kuhoji taarifa hizo wamezipata wapi na kwamba hilo jambo siyo sahihi na linachunguzwa ngazi ya CCM mkoa.

“Hili jambo lipo mkoani na vikao vinalifanyia kazi na halipo wilayani sasa wao wanapataje mamlaka ya kulizungumzia au kuna mtu anawatuma? Alihoji Hoja na kuongeza kuwa;
“Kwa nini wanaliingilia wakati lipo ngazi ya juu? Si wasubiri lifanyiwe kazi,” alisema Hoja.

No comments:

Post a Comment