Serikali ya Zanzibar yafurahia utendaji kazi wa Magufuli - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Sunday 5 November 2017

Serikali ya Zanzibar yafurahia utendaji kazi wa Magufuli

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema imeridhishwa na utendaji kazi wa Rais John Magufuli ambao unatokana na ushirikiano katika kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na viongozi wakuu waasisi wa taifa hili na kubadili hali ya uchumi ya Zanzibar.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed wakati akizungumza na gazeti hili kuelezea mafanikio ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Magufuli tangu alipochaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano baada ya ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka 2015.

Mohamed alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafaidika na ushirikiano mkubwa uliopo katika kipindi cha Rais Magufuli kwa kuendelea kutekelezwa miradi mbalimbali ikiwemo mfuko wa maendeleo ya jamii, Tasaf ,awamu ya tatu ambao unalenga kuzikomboa kaya masikini sana.

Alisema: ”Mfuko wa maendeleo ya jamii Tasaf awamu ya tatu ambao umelenga kuzikomboa kaya masikini sana kupiga hatua ya maendeleo ni mkombozi kwa wananchi wa Zanzibar ambao sasa umewawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika maendeleo na wengine kuziwezesha familia zao vizuri kupata huduma za kijamii ikiwemo Elimu.”

Kwa mfano, alisema zaidi ya kaya 33,632 zinanufaika na fedha zinazotolewa na Tasaf ambazo zipo zinazoihusisha jamii kupata fedha ambapo kwa upande wa Unguja ni kaya 18,944 wakati kaya za Pemba ni 14,688.

 ‘’Tasaf ni baadhi ya miradi inayotekelezwa kwa pamoja na Serikali zetu mbili kutokana na fedha za washiriki wa maendeleo ambao utekelezaji wake umeleta mafanikio makubwa na mabadiliko ukiwa na lengo la kuzikomboa kaya masikini nazo kushiriki katika maendeleo na kujikomboa na umasikini,”alisema.

Kwa mfano alisema katika kisiwa cha Pemba fedha za mfuko wa maendeleo ya jamii Tasaf zimesaidia katika sekta ya kilimo kwa kujenga tuta kubwa lenye urefu wa mita 200 na upana mita 8 huko Ndagoni Pemba ambalo limesaidia kuzuia maji ya bahari kuvamia mashamba ya wakulima.

Alisema kabla ya hapo zaidi ya wakulima 360 walishindwa kuendelea na shughuli za Kilimo baada ya maji ya bahari kuvamia mashamba ya kilimo na kusababisha athari kubwa za kimaumbile ambapo mabadiliko ya tabia ya nchi yanatajwa kuhusika moja kwa moja. ‘’Wananchi walitumia fedha za mfuko wa maendeleo ya jamii, Tasaf, kwa kuibua mradi wa kujenga tuta la kuzuwia maji ya bahari kuingia katika mashamba yao na hivyo kuendelea na kilimo chao ambapo kabla ya hapo tayari waliyahama mashamba yao,” alisema.

Aidha Mohamed ambaye ni msemaji mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alisema katika utendaji kazi Rais Magufuli amekuwa na ushirikiano mkubwa na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwashirikisha katika safari na misafara ya ziara ya njekwa niaba yake. 

’Tumeshuhudia mashirikiano makubwa yaliopo kati ya Rais Magufuli na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanzia Rais Ali Mohamed Shein na Makamu wa pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi katika safari za nje ambazo humwakilisha rais,”alisema.

Aidha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeridhishwa na utendaji kazi wa Rais Magufuli katika uwajibikaji wa watumishi serikalini, mapambano dhidi ya rushwa na ukusanyaji wa mapato kwa kuzitumia taasisi zilizopewa jukumu hilo. Kwa mfano alisema makusanyo ya kodi yameimarika kupitia Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kwa upande wa Zanzibar na hivyo kutoa nafasi kwa serikali kutoa huduma mbali mbali za jamii na kupunguza utegemezi wa misaada kutoka kwa wahisani. ‘

’Matokeo ya mapambano hayo tumeyaona kwa upande wa Zanzibar taasisi zinazokusanya mapato yameimarika na kuwepo kwa uadilifu mkubwa hatua ambayo imetoa nafasi kubwa kwa Serikali kutekeleza majukumu yake baada ya kupata makusanyo mazuri ya kodi.

No comments:

Post a Comment