Siri ya kiungo Haruna Niyonzima kushindwa kung'ara ndani ya kikosi cha Simba ni mfumo unaotumiwa na kocha, Joseph Omog.
Niyonzima amejiunga na Simba msimu huu lakini amekumbana na wakati mgumu klabuni hapo kwani katika mechi tisa za awali ameshindwa kung'ara jambo ambalo limeibua mijadala mikubwa juu ya ufanisi wa kiungo huyo mshambuliaji.
Hata hivyo tathmini inaonyesha kuwa hata Mohammed Ibrahim aliyekuwa akicheza katika nafasi hiyo kabla ya ujio wa Niyonzima, alitoa pasi moja tu ya bao katika mechi tisa za mwanzo za msimu uliopita.
Rekodi zinaonyesha kuwa mfumo wa Omog unatoa fursa kwa mabeki wa pembeni kutengeneza mabao mengi, huku viungo wakihusika zaidi katika kufunga jambo ambalo limemshinda Niyonzima aliyeifungia Yanga mabao sita tu Ligi Kuu katika kipindi cha miaka sita aliyoichezea.
Kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma alisema; "Wakati mwingine mfumo aliokuwa akitumia wakati akiwa Yanga unakuwa tofauti na alioukuta Simba, pia pengine kocha anampanga nafasi tofauti na aliyokuwa anaicheza akiwa Yanga."
"Mchezaji anaweza kuwa mzuri lakini kutokana na mabadiliko kama hayo anaweza asifanye vizuri sana, ni mjumuiko wa vitu vingi. Hili pia linategemea na mchezaji mwenyewe yuko vipi," alisema Djuma.
"Huwa inatokea mchezaji akitoka timu kubwa kwenda timu kubwa asianze vizuri, lakini anaweza kubadilika. Miaka pia inakwenda na inabadilika," alisema kocha huyo.
No comments:
Post a Comment