BEKI wa Simba, Shomari Kapombe ameibuka na kujibu tuhuma alizotupiwa na bosi wake, Zacharia Hans Poppe.
Hans Poppe juzi aliibuka na kumshushia lawama beki huyo kuwa amepona majeraha yake yanayomkabili na anakaa nje kwa uoga wake huku akiendelea kula mshahara wa bure wa kila mwezi tangu asajiliwe na Simba.
Beki huyo, tangu amejiunga na Simba msimu huu wa Ligi Kuu Bara kwa dau la shilingi milioni 35, hajacheza mechi yoyote kutokana na majeraha aliyoyapata akiwa na Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Akizungumza
Kapombe alisema yeye bado mgonjwa na haogopi kucheza kama anavyoeleza Hans Poppe kwani hakuna kipya kitakachomuogopesha.
Kapombe alisema, kwa mujibu wa daktari wake, atarejea uwanjani kucheza mechi za ligi kuu kwenye mzunguko wa pili akiwa fiti kabisa.
Aliongeza kuwa, kuhusiana na kuvunja mkataba wake, yeye hana tatizo kikubwa ni kufuata taratibu za kuuvunja.
“Unajua mimi ninashindwa kuelewa, ni jana (juzi) tu niliongea na Hans Poppe kwa njia ya simu na nikamuelezea tatizo langu, lakini nikashangaa kumsikia kwenye vyombo vya habari akinituhumu kuwa mimi siyo mgonjwa.
“Niseme kuwa, mimi bado mgonjwa nikiwa na maana sijapona vizuri kama anavyosema yeye, mimi nitaanza rasmi kuanza kuichezea Simba kwenye mzunguko wa pili wa ligi kuu nikiwa fiti kabisa.
“Sijaona kitu cha kuniogopesha mimi nishindwe kucheza, nikiwa Azam nimeichezea vizuri bila wasiwasi, kwa nini iwe Simba?” Alihoji Kapombe huku akibainisha kwamba kama Simba wanataka kuvunja mkataba wangu wafuate taratibu, wauvunje.
No comments:
Post a Comment