MTIBWA imeingia kwa mkwara mzito Dar es Salaam na kujinasibu kwamba hawaondoki burebure lazima kieleweke, lakini Simba wanacheeka wanawacheki tu na picha lote wanalijua.
Kocha wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila alisema; “Kwenye mechi yetu ya Jumapili watatusamehe kwani hatuwezi kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam kisha turudi bila pointi.”
“Hatuwezi kusafiri kwenda Dar es Salaam kisha turudi mikono mitupu, tunahitaji ushindi kwa namna yoyote ile na bila shaka vijana wangu watamshangaza mnyama,” alitamba kocha huyo.
Kocha wa Simba, Mkameruni, Joseph Omog alisema; “Nimewaona Mtibwa wakicheza na Yanga na walicheza vizuri jambo ambalo limenifanya kuwa na maandalizi ya umakini ili kutumia mapungufu niliyoyaona kupata matokeo ya ushindi katika mechi ambayo itakuwa na ushindani dakika zote tisini.”
“Ina wachezaji wengi wenye vipaji na wameanza vizuri msimu huu, kwahiyo mechi haitakuwa rahisi kabisa ingawa naendelea na maandalizi vizuri na wachezaji wangu ili kuibuka na pointi tatu ambazo tutaendelea kubaki kileleni,”alisema Omog.
“Itakuwa mechi ngumu, tutahitaji kupambana, unajua sisi tuliotoka Mtibwa na kujiunga na Simba, tunajua ubora na mapungufu ya timu hiyo,”alisema beki wa Simba, Salim Mbonde. Mtibwa itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kuing’ang’ania Yanga katika mchezo uliopita kwenye uwanja huo baada ya kutoka suluhu.
Hata hivyo rekodi zinaonyesha kuwa, Mtibwa Sugar wamekuwa wanyonge wa Simba kila zikikutana jijini Dar es Salaam kwani kwa misimu minne iliyopita imejikuta ikipokea vipigo mara zote.
No comments:
Post a Comment