MSHAMBULIAJI wa Simba John Bocco ‘Adebayor’ amesema atafurahi endapo atafanikiwa kuwafunga waajiri wake wa zamani wa Azam FC katika mchezo wa ligi kuu utakaofanyika kwenye uwanja wa Azam Complex keshokutwa Jumamosi.
Bocco alikuwa nahodha wa Azam kwa kipindi kirefu kabla ya mkataba wake kumalizika Julai mwaka huu na kujiunga na Simba ambapo Jumamosi atakutana na ‘ndugu’ zake hao kwa mara ya kwanza tangu aachane nao.
Bocco amesema hayo baada ya kumalizika kwa mazoezi ya jioni ya Wekundu hao yaliyofanyika katika uwanja wa Uhuru kuelekea mchezo huo ambapo alibainisha kama atapewa nafasi na kocha Joseph Omog ya kucheza atafurahi kuwafunga Azam.
“Itakuwa mechi ngumu, ila nikipewa nafasi na kocha Omog ya kucheza mchezo huo nitafurahi kuwafunga Azam kwakua mpira ni kazi yangu,” alisema Bocco.
Pamoja na kucheza muda mrefu katika uwanja wa Azam Complex, Bocco amesema ataingia kama mgeni ingawa hatapata ugumu wowote wa kutimiza majukumu yake.
Mbali na Bocco wachezaji wengine ambao watarejea katika uwanja wa Azam Complex wakiwa wapinzani kwa mara ya kwanza ni Aishi Manula na Erasto Nyoni huku Shomari Kapombe akishindwa kucheza kutokana na kuwa majeruhi.
Katika mchezo wa kwanza wa ligi ambao Simba iliibuka na ushindi mnono wa mabao 7-0 dhidi ya maafande wa Ruvu Shooting Agosti 26, Bocco alishindwa kucheza kutokana na kuwa majeruhi.
No comments:
Post a Comment