Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, amewajia juu baadhi ya watumishi wa serikali ambao wanatabia ya kuwafukuza kazi walimu wakuu wa shule ambao hutoa matokeo mabaya katika mitihani ya Taifa.
Ndalichako amesema hayo wakati akijibu hoja za wabunge kuhusu bajeti ya wizara yake na kuongeza watumishi hao hasa maofisa elimu, wanajukumu la kusimamia elimu katika eneo husika na sio kuwatupia lawama walimu pindi matokeo yanapokua mabaya.
“Hiyo sio sawa ni uonevu kwa wakuu wa shule kwa sababu na wenyewe wana viongozi juu yao, kwa nini wao ambao wanatakiwa kuwasimamia wasiwajibishwe, ninaagiza maofisa elimu wafanye kazi yao vizuri, utakuta mtu ana shule tano unashindwaje kuzisimamia, kwa hiyo katika hili serikali itahakiksha tunaimarisha usimamizi ikiwa ni pamoja na kuondoa viongozi ambao ni mizigo” amesema Ndalichako
Ndalichako ameongeza kwamba kama serikali inachukua hatua kubwa ili kuimarisha ubora wa elimu lakini baadhi ya watendaji hao wamekua wakirudisha nyuma jitihada hizo na serikali haitasita kuchukua hatua kwa watendaji hao.
Kwa upande mwingine Waziri Ndalichako ameitaka Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu (TCU) pamoja na Baraza la Taifa la Mafunzo ya Ufundi (NACTE) kuhakikisha wanafuatilia ubora elimu ya juu ili kutoa wahitimu wenye sifa zinazostahili na kiwango cha elimu husika.
No comments:
Post a Comment