KAMATI ya uendeshaji na usimamizi wa ligi, imemsimamisha mshambuliaji wa Yanga, Mzambia Obrey Chirwa pamoja na kiungo wa Tanzania Prisons, Lambart Sabianka kwa muda usiojulikana.
Wachezaji hao, wameadhibiwa kutokana na kosa la utovu wa nidhamu, walilolifanya kwenye mechi kati ya Tanzania Prisons na Yanga, iliyochezwa Novemba mwaka jana .
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura amesema, Chirwa pamoja na kiungo wa Prisons, Lambart Sabianka shauri lao limepelekwa kwenye kamati ya nidhamu ambayo itatolea uamuzi.
"Kamati baada ya kupitia ripoti ya kamishna wa mchezo, imebaini kwamba Chirwa na Sabianka wamefanya makosa ambayo yanakwenda kinyume na kanuni ya udhibiti na usimamizi wa wachezaji.Hivyo imeamua kuchukua uamuzi wa kuwasimamisha na kuwapeleka kwenye kamati ya nidhamu," anasema Wambura.
Hata hivyo mpaka sasa, Chirwa bado hajarudi nchini tangu alipokwenda kwenye mapumziko kwao Zambia.
No comments:
Post a Comment