WAKATI msanii Elizabeth Michael ‘Lulu’ akianza kutumikia kifungo chake cha miaka miwili jela kwa kosa la kuua bila kukusudia, wadau mbalimbali wanaonekana kumgeuzia kibao mama mzazi wa marehemu Steven Kanumba, Flora Mtegoa kufuatia kauli zake zinazotokana na hukumu hiyo iliyofanywa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Sam Rumanyika.
Katika kile kinachotafsiriwa kama furaha yake kufuatia hukumu hiyo, katika matukio mbalimbali Mama Kanumba amesikika akitoa maneno kama vile huu ni wakati wa wao (upande wa akina Lulu) nao kupata machungu kama ilivyokuwa kwake wakati kijana wake huyo alipofariki dunia.
Flora Mtegoa akiwa karika kaburi la Marehemu Steven Kanumba. Mama huyo ameonywa kuwa makini na kauli hizo kwani kibinadamu ni kauli ambazo hazifai kwa kipindi hiki ingawa alipotelewa mtoto wake. “Mimi namshangaa mama Kanumba, anakosea sana hata kama amefiwa angeonesha ubinadamu tu kwa sababu hata huyo Lulu aliumia kuondokewa na mpenzi wake.
Lile lilikuwa ni tukio la bahati mbaya, hakuna aliyependa litokee,” alisema msomaji aliyejitaja kwa jina la Sara. Mtu mwingine aliyekataa kutaja jina lake, alisema kwa kuwa Mama Kanumba ni mzazi, kwa busara angenyamaza tu kwani machungu aliyoyapata hata Mama Lulu naye ameyapata, japokuwa mwanaye hatorudi lakini ndiyo ashuruku Mungu kwani kwa upande mwingine Mungu amechukua mja wake kama ilivyoandikwa kwenye maandiko yake kuwa kina nafsi itaonja mauti.
“Mama Kanumba kama Lulu alimkosea angeshukuru tu akamuachia Mungu kuliko kuongea maneno hayo, akumbuke kuwa yule ni mtoto na mama yake ana machungu kama yeye alivyopata machungu,” alisema mwanamke aliyejitambulisha kama Mama Aisha.
Kauli nyingine ambayo imewakwaza watu ni pale alipodai kuwa hukumu hiyo imempa furaha kama wao walivyofurahia na kufanya sherehe ya kuzaliwa kwa mdogo wake Lulu, siku moja na ambayo yeye alikuwa akifanya kumbukizi ya kifo cha Kanumba.
Aidha, kauli nyingine ni ile aliyosema kuwa wakati wao walikuwa wakifika mahakamani kwa magari ya kifahari, yeye alikuwa akitumia usafiri wa daladala kwa shilingi elfu moja tu, kitendo kilichosababisha watu wamshushe.
Neno la Mhariri Kwa kuwa Lulu ameshahukumiwa kutumikia kosa alilolifanya, kwa busara kabisa Mama Kanumba sasa angetakiwa kukaa kimya kama alivyosema amemzika mwanaye rasmi, basi ashukuru kama alivyowahi kushukuru kwenye misiba mingine na kuamini kuwa Mungu ametenda.
No comments:
Post a Comment