ANATISHA……winga Simon Msuva ameendelea kuwaonesha ‘waarabu’ kuwa hawakukosea kumpa mkataba mnono baada ya hapo jana kucheza kwa kiwango cha juu na kuisaidia timu yake ya Difaa Hassan El Jadidi kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi FAR Rabat.
Mchezo huo wa ligi kuu nchini Morocco ‘Botola’ ulimaliza kipindi cha kwanza kwenye uwanja wa Prince Moulay Abdallah mjini Rabat, bila timu yoyote kuona lango la mwenzake.
Wenye waliingia kipindi cha pili kwa kasi na kufanikiwa kupata bao dakika 51 kupitia kwa Mohamed El Fakih ambalo lilidumu kwa dakika nne pekee kwani Bilal Al-Makri alifunga bao la kusawazisha kwa upande wa El Jadidi.
Muda mfupi baada ya mwamuzi wa akiba kuonesha dakika tatu za nyongeza, Msuva aliyeingia kipindi cha pili alipiga krosi safi iliyomaliziwa nyavuni kwa kichwa na straika Hamid El Ahadad na kuipatia timu hiyo ushindi muhimu wa ugenini.
Msuva amekuwa mchezaji muhimu kikosini hapo tangu asajiliwe akiifungia mabao muhimu timu yake pamoja na kusaidia upatikanaji wa mabao mengine.
No comments:
Post a Comment