Benchi la ufundi la Simba limefunguka kuwa baada ya kukwaa kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa sasa hawatakubali kung’oka kwenye nafasi hiyo hadi mwisho wa ligi ambapo watatwaa ubingwa kwa msimu huu.
Simba chini ya bosi wao mkuu, Joseph Omog walifanikiwa kurejea kileleni mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Stand United, na kufikisha pointi 11 wakiwa sambamba na Mtibwa Sugar na Azam, lakini wao wanaongoza kwa idadi ya mabao ya kufunga.
Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, amesema kuwa kwa muda mrefu walikuwa wanawaza kukalia usukani wa ligi ambapo baada ya sasa kupata nafasi hiyo watahakikisha wanashinda kwenye kila mchezo wao kwa ajili ya kuendelea kukaa kwenye nafasi hiyo na hawana mpango wa kushuka.
“Kiukweli tulikuwa tunataka tuwepo hapa tulipofika kwa sasa, yaani kuziongoza timu nyingine na hilo kwa sasa tumeshalifanikisha na tunachokipanga kwa sasa ni mbinu za kushinda kwenye kila mchezo wetu ujao.
“Ujue wakati tulipokuwa chini, mashabiki hawakuwa wanaelewa kwa sababu wanaona tuna kikosi imara kuliko hata wapinzani wetu wengine, lakini kwa sasa presha imepungua na tunaweza kufanya vizuri kwenye kila mchezo wetu kwa sababu tunacheza tukiwa na akili moja ya kushinda hapa ndiyo basi hatushuki tena,”alisema Mayanja.
No comments:
Post a Comment