KIUNGO mkabaji mpya wa Yanga, raia wa DR Congo, Pappy Kabamba Tshishimbi, ameanza na rekodi mbaya kwenye timu hiyo kwa kucheza mechi tatu huku akipewa kadi mbili za njano.
Tshishimbi alijiunga na Yanga msimu huu wa Ligi Kuu Bara akisaini mkataba wa miaka miwili akitokea Mbabane Swallows ya Swaziland.
Kiungo huyo mwenye rasta kichwani anayecheza namba sita, amepata kadi hizo katika mechi dhidi ya Lipuli FC iliyochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, nyingine ni dhidi ya Njombe Mji.
Hii ina maana kuwa kiungo huyo, anatakiwa kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu katika mechi nyingine zijazo za ligi kuu ili asipate kadi nyingine ya njano kwa kuwa ataukosa mchezo utakaofuata.
Kwa maana hiyo, kiungo huyo katika mechi hizo tatu alizozicheza alikosa kadi ya njano mchezo uliopita dhidi ya Majimaji ambao ulikuwa na presha kubwa ndani ya uwanja.
Ujio wa Tshishimbi ndani ya Yanga umekiimarisha kikosi hicho kutokana na kumaliza tatizo walilokuwa wakilalamikia muda mrefu tangu ameondoka kiungo wao Athumani Idd ‘Chuji’ ambaye
hivi sasa anaichezea Coastal Union inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Kiungo huyo, amedhihirisha ubora wake katika mechi za hivi karibuni ambazo amezicheza kwa kufanikiwa kuliziba pengo hilo katika mechi tatu za ligi kuu na ile ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar.
No comments:
Post a Comment