UMATI mkubwa wa watu ulitanda katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, kushuhudia kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita, Joseph Kasheku ‘Musukuma’, madiwani saba na mwananchi mmoja waliofikishwa mahakamani hapo jana.Musukuma na wenzake wanane wanakabiliwa na mashitaka manne ya jinai, likiwamo la kula njama.
Akiwasilisha mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Ushindi Swalo, mwendesha mashitaka wa serikali, Hezron Mwasinga, akisaidiana na Emil Kiria, alisema washitakiwa, kwa pamoja, Septemba 13, mwaka huu, majira ya saa nne asubuhi katika ukumbi wa Shirika la Maendeleo Geita (Gedeco) unaomilikiwa na Halmashauri ya Mji wa Geita, walipanga njama ya kuweka mkusanyiko usiokuwa na kibali, kuharibu mali na kuweka vizuizi katika barabara ya kuingia Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM).
Mbali na Musukuma ambaye pia ni Mbunge wa Geita, washitakiwa wengine ni Steven Werema (mkulima), Costantine Molandi, Winifrida Malunde, Ngundugu Joseph, Martine Kwilasa, Khadija Said, Maiko Kapaya na Maimuna Mengisi (wote madiwani).
Shitaka la pili, Mwasinga alidai linawahusisha watuhumiwa wanane kati ya tisa na alidai kwamba Septemba 14, majira ya saa 12 asubuhi katika kijiji cha Mtakuja, walifanya mkusanyiko usio halali.
Mwasinga alidai kuwa katika shitaka la tatu, Septemba 14, majira ya saa 12 asubuhi, washitakiwa hao wanane walitenda kosa la kufunga barabara ya kuingia na kutoka GGM na kusababisha wafanyakazi wa mgodi na watu wengine kushindwa kutumia barabara hiyo.
Katika shitaka la nne, Mwasinga alidai mahakamani hapo kuwa Septemba 14, majira ya saa 12 asubuhi, washitakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa la kuharibu bomba la maji katika kijiji cha Nungwe linalosafirisha maji kwenda GGM, hali iliyosababisha hasara ya Sh. milioni 12.25 na kupungua kwa huduma ya maji katika mgodi huo na kwa wananchi wa mji wa Geita.
Washitakiwa wote tisa kwa pamoja walikana mashitaka hayo huku mwendesha mashitaka wa serikali akiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa madai upelelezi haujakamilika.
Akiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 10, Hakimu Mfawidhi Swallo alisema dhamana kwa washtakiwa hao iko wazi na kila mmoja alitakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh. milioni tano.
No comments:
Post a Comment