Watu zaidi ya 100 wamefariki dunia baada ya ndege ya kuwabeba abiria aina ya Boeing 737 kuanguka na kulipuka karibu na uwanja mkuu wa ndege wa Cuba mjini Havana, katika mkasa mbaya zaidi wa ndege nchini humo katika miongo kadha.
Wanawake watatu waliondolewa kutoka kwenye mabaki ya ndege hiyo wakiwa hai, lakini taarifa zinasema wamo hali mahututi.
Ndege hiyo, ambaye iliundwa karibu miaka 40 iliyopita, ilikuwa imewabeba abiria 104 na wahudumu sita wa ndege.
Serikali ya Cuba imeanzisha uchunguzi, na kutangaza siku mbili za maombolezo ya kitaifa.
Ndege hiyo Boeing 737-201 ilianguka saa sita na dakika nane mchana Ijumaa, muda mfupi baada ya kupaa kutoka Havana.
Ndege hiyo ilikuwa kwenye safari ya ndani ya nchi kutoka Havana kwenda Holguin, mashariki mwa Cuba.
Wahudumu wote sita wa ndege hiyo walikuwa raia wa Mexico lakini wengi wa abiria ni raia wa Cuba.
Taarifa zinasema kulikuwa na abiria watano raia wa kigeni.
"Kumekuwa na ajali ya ndege ya kusikitisha sana. Taarifa tulizo nazo ni za kutamausha, yamkini kuna idadi kubwa sana ya waathiriwa," Rais wa Cuba Miguel Diaz-Canel alisema baada ya kutembelea eneo la ajali.
Ilikuwaje ndege hiyo ikaanguka?
Ni mapema sana kubaini chanzo cha ajali hiyo, lakini walioshuhudia kutoka ardhini wanasema ndege hiyo ilishika moto kabla ya kuanguka katika eneo wazi lililo karibu na msitu mbogo karibu na uwanja huo wa ndege wa Havana.
"Niliiona ikipaa," mfanyakazi wa duka la jumla Jose Luis aliambia shirika la habari la AFP.
"Ghafla, iligeuka na kuanguka. Tulishangaa sana."
"Tulisikia mlipuko mkubwa na kisha tukaona wingu la moshi ukitanda angani," Gilberto Menendez, ambaye ana mgahawa karibu na eneo la mkasa ameambia Reuters.
No comments:
Post a Comment